MICHONGO KAMILI

Saturday, 19 October 2013

YANGA VS SIMBA 20TH OCTOBER 2013

HIVI NDIVYO VIKOSI VYA SIMBA NA YANGA VITAKAVYO ZAMA DIMBANI LEO HII KUSAKA POINT TATU MUHIMU...



LANGONI…
Akianza Andrew Ntalla, au Abbel Dhaira kwa upande wa Simba SC, yeyote bado lango la Wekundu wa Msimbazi litakuwa kwenye mikono salama.  Kwa wote, hakuna kati yao aliyewahi kudaka timu hizo zikimenyana, lakini kabla ya kujiunga na Simba SC, wote wamekwishadaka dhidi ya Yanga, Ntalla akiwa Kagera Sugar na Dhaira akiwa Express ya kwao, Uganda. 
Lakini kwa kuwa tangu msimu umeanza Mganda, Dhaira ndiye amekuwa akisimama langoni mwa Simba SC, bila shaka kesho ataendelea. Huyu ni kipa mrefu mzuri na hodari wa kucheza krosi na mipira ya juu kwa ujumla na zaidi ana uzoefu wa kimataifa akiwa ameidakia Uganda mechi kubwa za mashindano makubwa- na ikumbukwe alikuja Simba SC akitokea Ulaya, alikuwa anadaka klabu ya Ligi Kuu Iceland, IVB.


 Upande wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ bila shaka ataanza na hiyo itakuwa mechi yake ya pili akiwa Jangwani kudaka dhidi ya Simba na ya tatu kwa ujumla katika mapambano ya watani, pamoja na ile aliyodaka akiwa Simba dhidi ya Yanga Aprili 19, mwaka 2009 timu hizo zikitoka 2-2.  Barthez ni kipa mzuri, ingawa siku za karibuni amekuwa akifungwa japo bao moja karibu katika kila mechi, ingawa mara nyingi hutokana na makosa ya mabeki wake. Lakini kwa sababu huu ni mchezo mkubwa, bila shaka Barthez atakuwa makini zaidi kesho akipangwa. Lakini hata ikitokea ‘bahati’ ikamuangukia Deo Munishi ‘Dida’ aliyesajiliwa msimu huu kutoka Azam, hapana shaka naye anaweza kufanya kazi nzuri.

SAFU ZA ULINZI:
Kwa Simba, Chollo bila shaka atacheza kulia, kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na katikati Kaze Gilbert na Joseph Owino, wakati kiungo wao mkabaji atakuwa Jonas Mkude au Abdulhalim Humud. Ukiondoa Mkude na Chollo ambaye kwa sasa ndiye Nahodha wa Simba SC, wengine wote katika safu ya ulinzi ya Simba ni wapya- Dhaira alikuwepo tangu Januari lakini hakucheza dhidi ya Yanga Mei mwaka huu na Owino amewahi kucheza Msimbazi msimu wa 2010/2011 baada ya hapo akawa nje kwa maumivu ya goti na alipopona akaenda Azam kwa msimu mmoja kabla ya kurejea kwao Uganda ambako amefufua makali na hatimaye msimu huu amerejea Simba SC. Humud amerejea Simba SC msimu huu baada ya misimu miwili ya kuwa Azam. Ukuta wa Simba SC uko madhubuti, ingawa mechi ya kesho ni kipimo chake kingine, tena kikubwa.
Kwa Yanga, Mbuyu Twite hapana shaka ataanza kulia, kushoto David Luhende, wakati katikati watakuwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan, kiungo wao mkabaji, Atjhumani Iddi ‘Chuji’.  Uzuri wa Twite zaidi ni katika kusaidia mashambulizi na kurusha mipira kama anapiga, ila kwenye ukabaji anapokutana na wachezaji wenye kasi na uwezo wa kumiliki mpira aina ya Ramadhani Singano, Twaha Ibrahim ‘Messi’ na Haroun Chanongo huwa uchochoro, lakini Luhende hakuna shaka atakaba vema na kusaidia mashambulizi pia.


 SAFU YA KIUNGO:
Kwa Simba SC, Mkude atacheza chini au Abdulhalim Humud, juu Said Ndemla au Amri Kiemba, pembeni kulia Twaha Ibrahim ‘Messi’ na Chanongo kushoto. Mkude, Humud tayari wote wazoefu wa mechi za watani na hakuna shaka yeyote kati yao ataiunganisha timu vizuri tu pale chini. Tofauti ya Ndemla na Amri Kiemba ni uzoefu tu, lakini kwa uwezo wa kuichezesha timu wote wazuri. Watu wa pembeni, Chanongo na Twaha wote wana kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kukimbiza, kupangua ngome. Wote wanaweza kufunga ingawa uzoefu unamfanya Chanongo awe zaidi ya Twaha. Ni matarajio Simba leo itashambulia zaidi kutokea pembeni. Mabeki wa Yanga watakuwa na kazi. Lakini pia kuna hatari makocha wa Simba wanaweza kujichanganya katika uteuzi wa kikosi cha kwanza, kwa sababu timu hiyo imesheheni viungo na mawinga wengi.       
Upande wa Yanga SC, Chuji atacheza chini, juu yake Frank Domayo, kulia Mrisho Ngassa na kushoto Haruna Niyonzima. Hakuna shaka juu ya Chuji pale chini na zaidi zile pasi zake ndefu kwa watu wa pembeni huzalisha mashambulizi vizuri sana. Domayo ni starehe tu kwa wana Yanga pale mbele na pembeni nako Ngassa ‘kama unanawa’, wakati Niyonzima japo hana kasi ya kulinganisha na mwenzake, lakini ni mtu anayefanya vitu vya uhakika. Ngassa kasi zaidi na Niyonzima uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, wote wanapangua ngome, wanapiga chenga na kufunga. Dhahiri mabeki wa Simba watakuwa na kibarua kizito kesho na kwa Niyonzima na Chollo yatakuwa marudio, ila Baba Ubaya na Ngassa ni picha mpya


SAFU YA USHAMBULIAJI: 
Kwa Simba Simba SC bila shaka Betram Mombeki ataanza pamoja na Amisi Tambwe. Hii ndiyo mechi ambayo Mombeki na Tambwe wanaweza kutengeneza heshima na si kwa kuwafunga Mgambo JKT. Mombeki ana uwezo wa kucheza mpira, nguvu na anaweza kufunga pia. Anakosa uzoefu tu wa mechi za watani kama mwenzake Tambwe. Lakini kama atatulia, kwa umbo lake na nguvu zake, amini Cannavaro na Yondan watalala na viatu. Upande wa pili, mtaalamu Tambwe yeye atakuwa anasoma tu pilika za Mombeki na mabeki wa Yanga kusubiri mpira utapotelea wapi, auwahi kuutumbukiza nyavuni. Tambwe ni mjanja sana na bila shaka kesho atakuwa mjanja zaidi, kwa sababu amekwishaambiwa kuhusu mechi za watani.
Kwa Yanga, ni Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza ndiyo wataanza kwa sababu ndiyo ambao wamekuwa wakicheza pamoja siku za karibuni. Wawili hawa ndiyo wafungaji wa mabao mawili yaliyopita Yanga SC ushindi wa 2-0 katika mchezo uliopita wa watani. Hizi mbili ni mashine na kwa hakika Kaze Gilbert na Owino wanatakiwa kufanya kazi haswa na si mzaha, vinginevyo watafuata nyayo za akina za Paschal Ochieng na Komabil Keita kuonyeshwa mlango wa kutokea Simba SC



 BENCHI;
Upande wa Simba SC, mbali na kocha Mkuu, Abdallah Kibadeni, msaidizi wake Jamhuri Kihwelo, kocha wa makipa James Kisaka, Meneja Nico Nyagawa na Dk Yassin Gembe, watakakuwepo Ntalla, Haruna Shamte, Adeyoum Ahmed, Hassan Isihaka, Humud, Ndemla, Ramadhani Singano, Sino Augustino, Edward Christopher, Rashid Ismail, Zahor Pazi na Marcel Kaheza. Abdallah Seseme hajaonekana kwa muda mrefu. Kuna uwezekano Kibadeni akawainua Singano na Edward kuongeza nguvu ya mashambulizi kipindi cha pili, ingawa Zahor Pazi ni mzuri zaidi, lakini damu yake haijaendana na makocha hao wote.  
Kwa Yanga SC, mbali na kocha mkuu Mholanzi, Ernie Brandts, Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro, kocha wa makipa Razack Ssiwa, Dk. Nassor Matuzya na Meneja Hafidh Saleh, watakuwepo Dida, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Job brahim, Salum Telela, Hamisi Thabit, Abdallah Mguhi, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Shaaban Kondo, Jerry Tegete, Hussein Javu na Said Bahanuzi.
Nizar ama, Msuva au wote na ama mmoja au wawili kati ya Tegete, Bahanuzi na Javu wanaweza kuchukua nafasi za watu kipindi cha pili.
Pamoja na ubora wa wachezaji, lakini mifumo na falsafa za uchezaji zitachangia sana matokeo katika mchezo wa kesho. Tumejionea katika mechi za karibuni, timu zote zinaweka mpira chini, unapitishwa kwenye njia zake mabao yanatafutwa kwa utengenezaji wa nafasi. Tumekwishatoka kwenye Simba na Yanga za enzi zile, ‘hakuna kuremba’ na sasa soka inachezwa.  Tunasubiri kuona makocha, mzalendo wa Simba SC, King Kibadeni na Mholanzi wa Yanga SC, Ernie Brandts wametuandalia nini siku ya kesho. Zaidi ya hapo, marefa tu wazingatie sheria 17 na wawe makini, mtu afungwe kihalali akalie na wachezaji wake. For the good of the game. Fair play.  

 

No comments:

Post a Comment

0653830825

Breaking News
Loading...

Search This Blog

LIKE PAGE ZETU ZA FACE BOOK

ZINGINE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...