Mmoja wa watu wanaosadikika watuhumiwa
wa matukio ya ugaidi nchini Kenya,Jihad Gaibon Swaleh, amefikishwa mahakamani
nchini Tanzania.
Mshukiwa huyo amesomewa mashtaka ya
kufadhili vitendo vya kigaidi nchini Kenya.
Pamoja naye watuhumiwa wengine 16
ambao wanadaiwa kuendesha vitendo vya kigaidi nchini Tanzania pia wamefikishwa
mahakamani hii leo wakikabiliwa na tuhuma za kula njama ya kutenda makosa ya
kigaidi nchini Tanzania.
Washtakiwa wote 17 wamerejeshwa
rumande baada ya kusomewa mashtaka ya vitendo vya kigadi nchini Tanzania pamoja
na nchi jirani ya Kenya.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na
mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali mwandamizi Prosper Mwangamila
ulidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kuwa kwa
kutumia mtandao wa facebook aliweza kushawishi watu wengine kuwasiliana kwa
lengo la kutafuta vifaa vya kulipua mabomu nchini Kenya na kusababisha
majerahi, hofu na Vifo.
Jihand Gaibon Swaleh ambaye
amesomewa mashtaka mawili hakuruhusiwa kukiri wala kukana mashitaka
yanayomkabili kutokana na kwamba mashitaka hayo yanaangukia katika makosa ya
ugaidi ambayo kwa mujibu wa sheria nchini Tanzania mahakama ya Hakimu Mkazi
haina mamlaka ya kuendesha kesi za namna hiyo.
Katika kesi ya awali kutajwa
mahakamani hapo washtakiwa wengine 16 walisomewa mashtaka mawili ikiwemo kula
njama kutenda kosa pamoja na kushawishi wenzao kushiriki katika vitendo vya
kigaidi katika sehemu mbali mbali nchini Tanzania.
Ni makosa ambayo wanadaiwa kutenda
kati ya Januari mwaka 2013 na Juni 2014 katika maeneo tofauti Tanzania.
Katika kesi zote mbili dhidi ya
washtakiwa hao Upande wa mashtaka uliiambia mahakama iliyokuwa chini ya hakimu
mfawidhi wa mahakama hiyo bi Hellen Riwa kuwa upelelezi bado unaendelea na
hivyo kuiomba mahakama kuahirisha kesi hizo hadi mwishoni mwa mwezi huu wa
Julai.
Awali mapema asubuhi msemaji wa
jeshi la polisi nchini Tanzania Bi Advera John Bulimba aliwealeza waandishi wa
habari kuhusu tuhuma dhidi ya washtakiwa hao
Hii ni mara ya kwanza kwa kundi
kubwa la watuhumiwa kufikishwa mahakamani kwa pamoja wakikabiliwa na tuhuma za
makosa ya kigaidi huku mtandao wa kijamii wa facebook nao ukitajwa kuhusika
katika kutawanya taarifa za kuwezesha kutenda makosa hayo.
THIS NEWS IS IN RESPECT OF BBC
SWAHILI…..