MICHONGO KAMILI

Tuesday 3 December 2013

Viongozi wa jumuiya ya afrika mashariki waliokutana mjini Kampla Uganda wametia saini sheria ya makubaliano ya kuwa na sarafu ya pamoja.



Kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kukuza mshikamano wa jumuiya hiyo yenye nchi tano.
Makubaliano hayo ya kisheria yalitiwa saini na viongozi wote watano wa jumuiya ya afrika mashariki kwenye kongamano la 15 lenye maudhui ya kuwa na sarafu moja.
Akizungumza kwenye kongamano hilo katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika mashariki bwana Richard Sezibera anasema kubuniwa kwa mkataba wa kuwa na sarafu moja ni hatua muhimu ya mshikamano haswa baada ya kuwa na soko la pamoja na umoja wa forodhani ambazo zinasaidia usafirishaji wa bidhaa na mitaji.
"Eneo letu linapiga hatua kubwa ya mshikamano haswa baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kuwa na sarafu moja. Umoja huu wa sarafu unaiweka jumuiya yetu kwenye awamu nyingine na ni hatua muhimu. Kutiwa saini kwa makubaliano Haya pia ni mwamko mpya wa mshikamanno wa kifedha."
Kutiwa saini kwa sheria hii ya sarafu moja kunatoa nafasi kwa nchi wanachama kuanza kuondoa sarafu zao za ndani ya nchi ili baadaye kuanza kutumia sarafu ya pamoja kote kwenye jumuiya ya afrika mashariki.
Mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo ambaye ni Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anaiona hii kama hatua muhimu ambayo itavutia zaidi wawekezaji kwenye eneo la afrika mashariki.
"Wafanyi biashara watapata Uhuru zaidi wakufanya shughuli zao huku nao wawekeaji wakiongezeka wakipata fursa bora ya kuja kwenye kanda hii. Tukiwa na manufaa kama hayo bila shaka uwekezaji utaongezeka na kuboresha uchumi wetu"
Chini yasheria hii nchi wanachama wa EAC wanatakiwa kuwasilisha sera zao za kubadilisha fedha kwenye benki kuu ya afrika mashariki itakayobuniwa, hii ikiwa ni hatua za kuelekea kuwa na sarafu ya pamoja.
Wajibu wa benki hiyo kuu ya afrika mashariki itakuwa ni kuthibiti dhamani ya sarafu moja na pia kusimamia maswala yote ya kifedha kwenye kanda.
Lakini ingawa viongozi wa afrika mashariki wanaisifu hatua hii ya sarafu moja na kuitaja kuwa yenye manufaa kwa mshikamano, wataalam wanahoji kwamba bado kuna maswala muhimu kuliko kuwa na umoja wa sarafu kama vile biashara baina ya nchi wanachama.
Bwana Louis Kasekende ni naibu gavana wa benki kuu ya Uganda.
"Sitaki tuzingatie kupita kiasi kuwa na sarafu ya pamoja. Lazima pia tuzingatie mambo ambayo tungependa kufanikishsa Kama vile maswala ya maendeleo ya kiuchumi. Tunahitaji kufanya biashara zaidi kwa kuuza bidhaa na huduma miongoni mwetu."
Lakini Gavana wa benki kuu ya Tanzania Profesa Benno Ndulu ana maoni tofauti.
"Tutakuwa tu na sarafi moja kwa hiyo inarahisisha sana biashara na inarahisisha pia kuwa na soko moja kubwa"
Tayari jumuiya ya afrika mashriki imefanikiwa kubuni soko la pamoja na umoja wa forodha hali ambayo imeimarisha biashara kufuatia kuondolewa kwa vikwazo vya barabarani na pia mipakani.
Nchi zote tano zina zaidi ya watu million 135 na kwa pamoja zina pato la jumla la dola bilioni 85.

Mkataba huu wa sarafu moja uliotiwa saini leo utatekelezwa ndani ya miaka kumi na hapo ndipo jumuiya ya afrika mashariki itaanza kutumia pesa moja tu.

No comments:

Post a Comment

0653830825

Breaking News
Loading...

Search This Blog

LIKE PAGE ZETU ZA FACE BOOK

ZINGINE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...